Mwanafunzi Chuo Kikuu auawa hosteli ya Mabibo, DSM
Mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bertha Mwarabu, amefariki dunia baada ya kuchomwa kisu tumboni na mwanafunzi mwenzake katika kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa mapenzi.
Bertha anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 23 na 24, alikutwa na mauti juzi usiku katika Hosteli za Chuo Kikuu Mabibo, baada ya kushambuliwa kwa visu kadhaa mwilini hasa tumboni na mwanafunzi mwenzake wa DUCE, Masamba Musiba anayedaiwa alikuwa ni mpenzi wake wa muda mrefu.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, Mark Kalunguyeye alithibitisha jana kwa simu kutokea kwa mauaji hayo na wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa upelelezi na kwamba atapelekwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni ya Mwananyamala.
Kwa mujibu wa wanafunzi wenzake wakiwamo marafiki wa karibu wa marehemu, Bertha na mtuhumiwa walianza mapenzi muda mrefu tangu wakiwa wanafunzi wa shule mkoani Morogoro. Inaelezwa kuwa tangu waanze masomo chuoni hapo, uhusiano wao haukuwa mzuri kutokana na ugomvi wa mara kwa mara huku chanzo kikubwa kikidaiwa ni tabia ya ulevi aliyokuwa nayo mvulana ambayo mwenzake alichukizwa nayo.
Wote walikuwa mwaka wa pili DUCE. “Mara nyingi Bertha alikuwa akilalamikia tabia ya mpenzi wake huyo kutokana na ulevi, na kusema kuwa ipo siku ataachana kabisa na mpenzi wake huyo endapo ataendelea na tabia yake ya ulevi,” alisema mwanafunzi ambaye ni rafiki wa marehemu, lakini kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.
Kwa mujibu wa rafiki huyo, Bertha alimpa mpenziwe mwezi mmoja wa kujirekebisha kutokana na tabia hiyo na kumtishia kusitisha uhusiano wao endapo angeendelea na tabia hiyo, lakini pamoja na hilo mpenzi wake huyo hakujirekebisha na ndipo msichana akachukua uamuzi wa kusitisha uhusiano huo.
Kwa mujibu wa mashuhuda katika Hosteli ya Mabibo ambao ni wanafunzi wenzao, tukio hilo la mauaji lilitokea saa tatu usiku katika makazi ya msichana huyo ambayo ni Jengo la Block C, chumba namba 250, ambacho kilikuwa na vitanda vinne kikiwamo cha Bertha. Inaelezwa kuwa msichana huyo alirejea chumbani kwake majira ya usiku akitokea matembezini na inaaminika kuwa alikuwa anatokea kanisani; na aliingia chumbani kwake akiwa na chakula mkononi.
Inaelezwa kuwa alikiweka ndani na kutoka nje ya chumba kwenda kuitikia mwito wa mpenzi wake huyo ambapo kwa muda huo alikuwa akimsubiri nje ya chumba alichokuwa akiishi msichana huyo. Lakini bila kutambua mauti yatamfika, ghafla inaelezwa na mashuhuda ambao ni jirani, mvulana huyo alimvamia Bertha na kuanza kumchoma visu tumboni, hali iliyowafanya waogope na kujifungia ndani huku wakipiga kelele kuomba msaada kwa watu wengine.
“Tulishuhudia akimchoma visu tumboni hali iliyotufanya tuogope na haraka tukarudi chumbani na kuanza kupiga kelele za kuomba msaada,” alisema msichana mmoja jirani wa Bertha. Inaelezwa baada ya tukio hilo, mvulana huyo alikwenda chumbani kwake na kuchukua begi lake dogo na kuanza kukimbia kwenda nje ya hosteli hiyo; huku wasichana walioshuhudia tukio hilo wakianza kupiga kelele za kuwataka watu wamkamate mvulana huyo aliyekuwa akitaka kupanda uzio ili aruke nje.
Awali, wanafunzi waliokuwa nje walimkamata na kuanza kumpiga wakijua ni mwizi ambapo baadhi walimtambua kuwa ni mwanafunzi mwenzao na ndipo wakati wakijiuliza kafanya nini, ndipo taarifa kutoka ndani, zilifika zikimhusisha na tukio hilo la kumchoma kisu mwanafunzi mwenzake.
Baada ya kukamatwa na askari wanaolinda jengo hilo, alipelekwa katika Kituo cha Polisi Kimara ambako anashikiliwa na Polisi, na msichana huyo anadaiwa alipelekwa kwenye zahanati katika hosteli hizo kabla ya kukimbizwa hospitali, lakini inaaminika alifia njiani. Kutokana na tukio hilo, rafiki yake wa karibu wa Bertha, Fausta Mushi amepatwa na wakati mgumu kwa kupoteza fahamu, kila anapokumbuka tukio hilo kwani aliachana na rafiki yake muda mfupi kabla ya ajali hiyo na kwenda chumbani kwake. Amelazwa katika Zahanati ya Chuo Kikuu, sehemu ya Mlimani - http://www.habarileo.co.tz
0 feedback :