wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Monday, May 18, 2009

TweetThis! Mramba & Yona wafutiwa shitaka (mojawapo)

UPANDE wa mashitaka katika kesi inayowakabili waliokuwa mawaziri waandamizi wa Serikali ya awamu ya tatu, Bw. Basil Mramba (Wizara ya Fedha) na Bw. Daniel Yonna wa (Nishati na Madini) umebadili hati ya mashitaka na kuwaondolea shitaka moja.

Mabadiliko ya hati hiyo yalitakiwa kwenda sambamba na usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo ambao ulikwama baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka kupewa nakala za maelezo hayo zikiambatana na nyaraka mbalimbali zinazotarajiwa kutumika kama vielelezo.

Hayo yalifanyika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya jopo la Mahakimu watatu ambao, ni Bi. Fatuma Masengi, Bw. John Utamwa na Bw. Saul Kinemela.

Upande wa mashitaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Boniface Stanslaus, uliiomba mahakama hiyo kubadili hati ya mashitaka ya washitakiwa hao ambayo awali ilikuwa na mashitaka 12 hivyo kuondoa shitaka la tano na kufanya mashitaka hayo kubaki 11.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa mwingine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bw. Gray Mgonja ambapo shitaka lililoondolewa na upande huo, lilihusiana na washitakiwa hao kukaidi ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kutoiondolea kodi Kampuni ya M/S Alex Stewart shitaka ambalo limeelezewa katika mashitaka mengine.

Baada ya upande wa mashitaka kubadili hati hiyo kwa kuondoa shitaka hilo uliiomba Mahakama kusoma maelezo ya awali ya washitakiwa hao hali iliyokwamishwa na maombi ya upande wa utetezi.

Upande wa utetezi uliowakilishwa na Prof. Leonard Shaidi uliwasilisha ombi la kutaka nyaraka zitakazotumika katika kesi hiyo ziambatanishwe na nakala za maelezo ya washitakiwa hali iliyopingwa vikali na upande wa mashitaka.

Akiwasilisha ombi hilo, Prof. Shaidi alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 192(4) cha CPA kinatoa maelekezo ya namna ya kupewa nyaraka hizo.

Akipinga hoja hiyo, Bw. Stanslaus, alisema kuwa sheria haiwahitaji wao kama upande wa mashitaka kutoa nyaraka hizo kwa upande wa utetezi hivyo hawaoni sababu ya kufanya hivyo.

"Sheria iko wazi kuwa nyaraka ambazo zitakuwa hazina ubishani kwa pande zote mbili zitakuwa hazina sababu ya kuitiwa ushahidi na kwa zile zitazokuwa na ubishani ndizo zitatolewa ushahidi na nyaraka hizo zinaweza kuwasilishwa hata kama kesi inaendelea," alisema Bw. Stanslaus.

Akizungumzia nakala za maelezo ya awali, aliiomba Mahakama kuwapa muda ili kuandaa nakala za kutosha kwa pande zote mbili.

Kwa upande wa mahakama ilisema kuwa kutokana na malumbano makali ya kisheria jopo linaona ni busara kupata muda wa kwenda kupitia kwa makini vifungu vya sheria ili kufikia uamuzi wa haki hivyo uamuzi kuhusiana na maombi hayo ya nyaraka utatolewa Alhamisi mahakamani hapo.

Awali washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakidaiwa kuwa kati ya Agosti 2002 hadi Juni 2004 mshitakiwa Bw. Mramba na Bw. Yonna wakiwa mawaziri katika wizara zao, walitumia madaraka vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha shughuli za madini na Kampuni ya M/S Alex Stewart ya Uingereza na kampuni zingine ndogo kutoka kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Walidaiwa kuwa Mei 28,2005 walisaini mkataba wa kuongeza muda wa uzalishaji wa madini na kampuni hiyo kinyume na sheria ya manunuzi na madini.

Walidaiwa kuwa kati ya mwaka 2003 hadi 2005 wanadaiwa kuidhinisha vibali vyenye namba 423, 424, 497,498,377 na 378 vya kuiondolea kampuni ya M/S Alex Stewart kodi katika kazi za uzalishaji wa madini.

Shitaka la mwisho, linawakabili washitakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa kati ya kipindi cha mwaka 2003 hadi 2005, kwa kutumia vibaya madaraka yao, waliisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7 - Grace Michael, Majira

0 feedback :

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads