wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Tuesday, January 06, 2009

TweetThis! Kiharusi (Stroke)

Mwaka 2005 nikiwa Iringa nilikuwa nazungumza na rafiki yangu ambaye alikuwa akinisimulia mikasa aliyowahi kukumbana nayo katika gurudumu la maisha. Rafiki yangu huyu alinifahamisha suala moja ambalo kama kawadia ya watu wengi, aliamini kuwa alikuwa amelogwa na (m)wanakijiji fulani. Aliamini hivi kwa kuwa hali ya kustaajabisha ilimtokea alipokuwa kwenye sherehe, ghafla aliona utando machoni na hali ya kiza, alihisi kupoteza fahamu, mwili ulimwisha nguvu na alishindwa kabisa kusikia ama kufuatilia maongezi ya watu karibu yake. Kutonana na hali hiyo, ghafla alikwenda kwenye gari yake, akaipasha moto na kushika njia kuelekea nyumbani. Anasema kuwa hakumbuki alivyowea kuendesha gari hadi kufika nyumbani lakini anachokumbuka ni kuwa aliibuka akajikuta kitandani akihudumiwa na watu anaoishi nao na ndipo alipogundua kuwa amepoteza nguvu katika sehemu ya kushoto ya mwili wake (kwa bahati mbaya yeye ni 'mashoto') hivyo ilikuwa rahisi sana kufahamu kuwa amepoteza nguvu yake.

Nilipomaliza kumsikiliza, nilimfahamisha kuwa, nadhani hiyo haikuwa imetokana na ulovi bali ni hali ya kupatwa na kiharusi na ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu kuwa alikuwa hai kwani asilimia karibu sitini ya watu wanaopatwa na dalili kama alizonihadithia, huishia kupoteza uhai.

Kwa bahati nzuri, rafiki yangu alikwenda Ulaya na kupata huduma ya uchunguzi na utabibu na hatimaye alipewa dawa pamoja na maelekezo ya vipimo ili kujikinga na hatari za kupatwa na kiharusi kwa mara nyingine. Tangu wakati huo, amekuwa akizingatia masharti na maelekezo yote na sasa ni mwaka wa nane vipimo vinaonesha kuwa madhara yaliyotokana na kiharusi yamedhibitiwa.

Je, wanaposema 'kiharusi' humaanisha nini hasa?
Mara nyingi kiharusi husababishwa na damu yenye oksijeni kushindwa kupita katika mishipa ya damu, yaani ateri, katika kusafirisha damu kwenye viungo muhimu mwilni kama vile ubongo. Hali hii inapotokea, sehemu fulani ya ubongo huwa imenyimwa uwezo wake wa asili wa kufanya kazi na hivyo hufa. Inapotokea sehemu fulani ya ubogo kufa, ndipo viungo vyote vya mwili vinavyopokea maelekezo kutoka kwenye sehemu iliyokufa ya ubongo, hushindwa kufanya kazi kwa kukosa maelekezo. Kwa mfano, mtu aliyeathirika sehemu ya kulia ya ubongo, hupoteza uwezo wa kutumia mkono ama mguu ama mdomo wa kushoto na mdomo kupinda upande wa kushoto na pengine kushinda kabisa kuzungumza.

Madhara yaliyotokana na hali hii yanaweza kuwa ni ya muda mfupi ama muda mrefu vile vile yanaweza kuwa maharibifu nusu kwa maana kuwa sehemu tu ya kiungo imedhurika ama maharibifu kamili kwa maana kuwa sehemu nzima ya kiungo imeharibika.

Watafiri na wataalamu mbalimbali wa nyanja za afya wamegundua kuwa, ikiwa mtu aliyepatwa na kiharusi atawahishwa hospitalini na kupewa matibabu ya haraka baada tu ya dalili za kiharusi kuonekana, upo uwezekano mkubwa wa kuiwezesha damu kurudia katika mtiririko wake wa kawaida ndani ya ubongo na hivyo kupunguza uwezekano wa kusababisha madhara makubwa.

Jinsi ya kuzitambua dalili za kiharusi
Ikiwa utaziona dalili mojawapo ama zaidi ya hizi zifuatazo, fanya hima kuwafahamisha watu watakaoweza kukusaidia kuwahi matibabu hospitalini ama kwa mganga haraka. Dalili hizo ni:
 • Ghafla kuishiwa nguvu na hisia usoni, mkononi au mguuni katika upande mmoja wa mwili.
 • Ghafla kuona utando ama kiza machoni au kutokuona kabisa (hata ikiwa ni jicho la upande mmoja tu).
 • Kupoteza kauli, kupata shida wakati wa kuzungumza, kutokupata uelewa ama kufuatilia mazungumzo ya kawaida ya watu unaozungumza nao kwa wakati huo.
 • Maumivu ya kichwa ya ghafla yasiyo na chanzo.
 • Kizunguzungu, kujihisi kuishiwa nguvu mwilini, kuanguka, ama kutokuweza kuwa na stamina wakati wa kutembea.
 • Ama, dalili nyingine ya kiharusi hufahamika kwa jina la kitaalamu kama 'Transient Ischemic Attack (TIA)' ambayo ni sawa na 'nusu kiharusi', kwa maana ya kwamba, TIA haina madhara makubwa kama yale yanayotokana na kiharusi. Hata na hivyo, mtu anapopatwa na TIA hatakiwi kuzembea katika kuchukua hatua za haraka kufika hospitalini kuonana na mganga ama mshauri wa afya kwa uchunguzi zaidi.
Kuvifahamu vichocheo vinavyoweza kusababisha kupatwa na kiharusi
Mtu mwenye moja au zaidi ya mambo yaliyotajwa hapa chini, anaweza kuwa katika kundi la hatari ya kupatwa na kiharusi:
 • Kuzaliwa katika familia ambayo baba au mama (pia bibi au babu) alimewahi kupatwa na kiharusi.
 • Lehemu/mafuta mengi na yanayoganda kwenye mishipa ( cholesterol) kwenye mishipa ya damu (hutokana na kula vyakula vyenye mafuta mengi)
 • Kisukari kisichotibiwa.
 • Shinikizo kubwa la damu.
 • Uvutaji sigara.
 • Kupatwa na TIA wakati wowote.
 • Magonjwa ya moyo.
 • Kutambulika kuwa una ugonjwa wa mishipa ya ateri ya karotidi (mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo) - carotid artery.
Kanuni ndogo za jinsi ya kujiepusha na kiharusi

 • Soma na jadiliana na mganga kuhusu hatari ya kupatwa na kiharusi ikiwa una mojawapo ya vichocheo vilivyotajwa hapo juu.
Mambo mengine ya kuzingatia ni pamoja na:
 • Kufuata ushauri na maelekezo ya mganga ikiwa una shinikizo la juu la damu.
 • Epuka kula vyakula vyenye mafuta na chumvi nyingi (ili kupunguza wingi wa lehemu na shinikizo la juu la damu).
 • Ikiwa una kisukari, hakikisha unazingatia maelekezo juu ya matibabu.
 • Zingatia kiwango cha pombe/kilevi unachotumia kulingana na afya yako.
 • Acha kuvuta sigara. Ikiwa huvuti sigara, usishawishike kuanza kuvuta sigara.
 • Wasiliana na mganga ama mhudumu wa afya kuhusu ushauri wa kubadili na kuwa na mwenendo afiki wa kimaisha.
 • Usisite kutaka ushauri kutoka kwa marafiki, ndugu pamoja na jamaa wanaoweza kuwa na ufahamu zaidi juu ya kiharusi ama masuala ya afya.
 • Zingatia kufanya uchunguzi wa afya wa mara kwa mara juu ya mwenendo wa afya yako hasa pale unapohisi kuwa katika hatari ya kupata TIA ama kiharusi.
 • Aina fulani ya Aspirin inayojulikana kama 'baby aspirin' (81mg) huweza kusaidia damu isigande na hivyo kuweza kuzunguka kwa urahisi zaidi kwenye mishipa ya damu.
Inakisiwa kuwa kwa wastani, watu wapatao milioni 12 hupoteza uhai kutokana na kiharusi. Hii huwakumba zaidi wanaume walio na umri wa kuanzia miaka 55 ama kabla ya hapo ikiwa mtu atakuwa katika kundi lenye vichocheo vya hatari vilivyotajwa hapo juu.

Rejea nilizotumia wakati wa uandaaji wa somo hili:
 1. WHO - Avoiding Heart Attacks and Strokes.pdf (the eBook also available)
 2. Family Doctor - Stroke and common heart diseases

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads