wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Saturday, November 22, 2008

TweetThis! Hali ya kuwa albino

Kutokana na habari za kusikitisha za ukatili unaofanywa na watu fulani fulani kwa jamii ya albino Tanzania, nimeona vyema kuandika japo kwa ufupi juu ya hali ya kuwa albino hili.

Watu wa jamii ya ualbino wanazo haki zote alizonazo binadamu mwingine yeyote na zaidi wanastahili msaada wa kipekee wa kibinadamu kila wanapohitaji, ili kuweza kuyakabili maisha na kuikubali hali ya utofauti waliyozaliwa nayo ambayo kwa hakika hawakuichagua, bali kujikuta wamezaliwa hivyo.

Hali ya kuwa albino?
Hali ya ualbino hutokana na upungufu ama ukosekanaji kabisa wa kiasi fulani cha protini katika mwili ambacho hutakikana katika utengenezaji wa rangi ya ngozi, wataalam huita - melanin. Ualbino huweza kuwakumba binadamu, wanyama na mimea.

Ualbino unavyotokea
Hali ya ualbino wa kuzaliwa huonekana tangu mtoto anapozaliwa kwa kurithi chembechembe za uzazi (gene) kutoka kwa wazazi wawili kwani 'gene' hizi huwa zimejificha (reccessive genes) katika mbegu za baba na mayai ya uzazi ya mama.
Tatizo la kukosekana kwa melanin ya kutosha hutokana na mabadiliko (mutation) yaliyotokea katika kichocheo (enzyme / catalyst) cha 'tyrosinase' ambacho hutakiwa kuchochea na kuhakikisha kuwa hatua ya mwisho ya utengenezaji wa melanin kutoka kwenye protini ya 'tryrosine' umekamilika.
Kwa hivi:
Tyrosine + tyrosinase = IPO Melanin (rangi ya kawaida)
Tyrosine - tyrosinase = HAKUNA Melanin (albino)
Ukosekananji ama upungufu wa melanin mwilini husababisha kubadilika rangi ya ngozi, nywele na macho.

Ni kwa nini iwepo tofauti katika watoto wa baba na mama mmoja?
Sababu ya tofauti kati ya watoto kuzaliwa wenye rangi ya ngozi ya kawaida na wale wenye upungufu wa melanin hutokana na 'genes' alizorithi mtoto kutoka kwa wazazi wake. Hivi ni kusema kuwa, ikiwa baba na mama wana 'genes' za albino, basi wakati wa kutunga mimba ikatoka mbegu moja ya baba yenye ualbino ikalirutubisha yai la mama lenye ualbino, mtoto atakayezaliwa kutokana na muunganiko huo atakuwa albino. Katika uzazi unaofuatia, ikiwa mbegu ya baba isiyo na ualbino itatoka na kulirutubisha yai la mama lisilo na ualbino, mtoto atakayezaliwa hatakuwa albino bali atakuwa na ngozi yenye rangi ya kawaida. Kwa ufupi, bila njia ya kitaalamu kuchunguza mbegu/mayai ya uzazi, ni vigumu kwa hali ya kawaida kutanabahi kuwa mbegu/yai litakalopevushwa lina ualibino ama la.

Hapo awali nimesema kuwa 'gene' hizi ni 'recceccive' hivyo hazina nguvu na wala si nyingi ikilinganishwa na 'gene' zilizobakia yaani 'dorminant genes', kwa maana hiyo, inawezekana kabisa kuwa mtoto akazaliwa na hali ya ualbino-chotara. Yaani hali yake ya ngozi inaonekana kama vile "si albino wala si kawaida". Muonekano wa ngozi yake ni wa mng'ao wa tofauti. Hii itatokea endapo, itatoka mbegu ya baba yenye ualbino ikawa na nguvu (dorminant gene) na kulirutubisha yai la mama lisilo na ualbino; ama, likarutubishwa yai albino la mama (dorminant gene) kwa mbegu isiyo albino ya baba. Kwa ufupi:
Mbegu albino dorminant + Yai kamili = Chotara-albino
Mbegu kamili + Yai albino dorminat = Chotara-albino

Hapo awali pia niliandika kuwa, ukosefu wa melanin huathiri macho na hii ndiyo sababu hasa ya tatizo la albino kupepesuka/kuwewesua macho (photophobia). Melanin hutakiwa kwa kiasi cha kutosha katika sehemu ya jicho inayohusika na kurekebisha mwanga, yaani retina, kabla ya kuutuma kwenye sehemu ya ubongo inayohusika na kutafsiri aina ya rangi na ukali wa mwanga. Melanin inapokosekana ama kupatikana kwa uchache, huisumbua na kuisababisha retina ishindwe kufanikisha kazi yake kisawasawa na hivyo kuweweseka katika hali ya kutaka kuikamilisha kazi yake. Mweweseko huu ukiwa na nguvu sana kwa mfano, kutizama kwenye mwanga mkali kwa muda mrefu, huweza kulegeza misuli ya macho na kusababisha kichwa kuuma. Ili kupunguza tatizo hili, ni vyema albino wakavaa miwani za kukinga macho kutokana na mwanga mkali wa jua ili kulipunguzia jicho kazi ya ziada.

Nilizungumzia pia juu ya athari ya kutokuwepo kwa melanin kwenye ngozi ambapo albino huwa katika athari ya kupata magonjwa na kansa ya ngozi inayotokana na miale mikali ya jua (ultra violet light - UV light) ndiyo maana, albino wengi hawana budi kutumia vifaa vitakavyowakinga na jua kali. Mfano, kutumia mafuta maalumu yaliyotengenezwa kwa ulinzi wa ngozi (sun screen/protection cream) ama vitambaa/khanga, miavuli na vile vile kutembea katika maeneo yenye kivuli kila inapowezekana.

Ni rahisi kwa albino ama wazungu kupata kansa ya ngozi kwa kuwa hawana melanin ya kutosha kusharubu na kupambana na ukali wa joto la jua. Nimewahi kusikia na kuwaza kuwa, pengine hii ndiyo sababu ya wazungu kulalamika kuwa wao joto haliwasumbui kwa kuwa ati ni kali bali ni kwa vile linawaletea kansa ya ngozi, yaani ngozi zao huakisi mwanga tofauti na watu wenye ngozi nyeusi ambayo husharubu joto. Yaani kwa ngozi yenye melanini ya kutosha, joto kali linachoma hadi kuleta hisia ya kuungua ama kufuka moto ndani kwa ndani.

Je, ualbino unaweza kumpata mtu katika umri mkubwa?
Kama nilivyoandika hapo awali, ualbino uliozoeleka zaidi ni ule wa kuzaliwa. Lakni pia, upo ualbino unaotokea ukubwani na huu husababishwa na matatizo ya ngozi kuchubuka wataalamu huita 'vitiligo'. Hali hii hutokea kwa watu ambao miili yao huanza kupoteza melanin kutokana na mabadiliko (mutation) yasiyozuilika.

Nukuu na rejea nilizopitia wakati wa kuandika:
eMedicine article by Raymond E Boissy, PhD
Science on Albinism

0 feedback :

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads