wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Monday, July 20, 2009

TweetThis! Tanzania tuna mjusi wa historia huko Ujerumani! Ivo kumbe eeh?

Ama kweli kuishi kwingi kama si kusikia mengi, basi ndiko kuona mengi. Leo hii rafiki yangu mmoja ameniorodheshea mali asili tuliyonayo Tanzania na kuniacha mdomo wazi. Aliyoyataja ni mengi na miongoni mwa hayo, mengine yamenifanya kujiuliza ikiwa kweli ninaifahamu vilivyo historia na jiografia ya nchi yangu.

Sasa tena nikiwa napekua pekua magazeti, nikashangazwa na hii habari ya mjusi wa kihistoria kutoka mkoani Lindi nchini mwetu hapa hapa Tanzania ati yupo huko Ujerumani. Nimejaribu sana kukumbuka kama mwalimu wa Shule ya Msingi hadi Sekondari aliwahi kulitamka hili, kwa kweli kumbukumbu zangu zinanikatalia, na kwa bahati mbaya sina hata chembe ya ugonjwa wa kusahau, lau kama nimesahau, basi vitabu vya kiada haviwezi kuwa vimekosea, sasa iweje hata nisisikie mtu anasema kuhusu huyu mjusi? Na siwalaumu Walimu wangu. Wao wangejuaje? Ah, potelea mbali, popote alipo, huyo ni mjusi wetu.

Swali ninalojiuliza bila  ya kuwa na majibu ya kukidhi haja ni je, hiyo siku ya kiama (kama ipo) tutakapoulizwa WaTanzania utetezi wetu wa ni kwa nini tuliishi kimasikini (ingawaje wapo wachache miongoni mwetu wanaoogeleka kwenye ukwasi), tutatoa maelezo gani? Mi nimefikiri kwa kukurupuka nikasema, nitajitetea 'Si ni hao Viongozi uliotupa?' lakini nikajiuliza, kama akiambia, 'si ni ninnyi mliwachagua wenyewe?', hapo nitamjibu kauli gani? Aliyepiga kura, Asiyepiga kura, wooote manzanyaze! Sote tu lawamani.

Habari ya mjusi ndiyo hii, kama ilivyo andikwa na Na Kizitto Noya toka Dodoma na kuchapishwa na gazeti la Mwananchi.
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe ametofautiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga kuhusu kurudishwa nchini kwa mjusi mwenye urefu wa mita za mraba 22 (dinosaur) aliyechukuliwa na Wajerumani mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Wakati Waziri Membe akisema mpango wa serikali kumresha mjusi huyo nchini bado thabiti, Mwangunga alisema serikali inaangalia kama kuna uwezekano huo ama kumwacha mjusi huyo nchini Ujerumani. Hata hivyo, Waziri Mwangunga alieleza ingawa jambo hilo bado linaangaliwa kwa makini, ni bora mjusi huyo akabaki Ujerumani kupunguza gharama za maandalizi ya kumleta na kumhifadhi nchini. Alisema serikali inatakiwa kujenga jengo la ghorofa tatu kwa ajili ya kumhifadhi mjusi huyo aliyechukuliwa nchini enzi za ukoloni kati ya mwaka ya 1918 na 1919 kutoka Kijiji cha Mipingo mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa Waziri Mwangunga, mjusi huyo anaweza kuendelea kubaki Ujerumani na Tanzania kukusanya mapato yatokanayo na mjusi huyo akiwa huko kwani gharama za kumrudisha nchini ni pamoja na kubomoa mifupa yake, kuisafirisha na kuiunda upya. “Tunajaribu kuangalia kama kuna umuhimu wa kumrudisha mjusi huyo ama abaki Ujerumani, alisema Mwangunga akijibu swali la Mbunge wa Masasi (CCM), Raynald Mrope.

Mrope alitaka kujua sababu za Serikali kuchelewa kumrudisha mjusi huyo kama ilivyoshauriwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi Elimu na Utamaduni (UNESCO) baada ya serikali ya Ujerumani kuendelea kukusanya mapato mengi kutokana na mjusi huyo.

Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema, uamuzi wa kurudisha mifupa ya mjusi huyo bado upo na serikali imeiandikia nchi ya Ethiopia kuomba wataalam wa kumsafirisha. “Nchi ya Ethiopia iliunda kamati iliyofanikisha kurudisha nguzo za kihistoria nchini humo,” alisema Membe akielezea wanachama wa kamati hiyo wanaweza kushirikiana na Tanzania kuona namna ya kumrudisha mjusi huyo.

1 feedback :

Mzee wa Changamoto said... Mon Jul 20, 11:48:00 AM MST  

Here we go again. What a stupid idea waliyonayo hawa wenzetu kuwa wanaweza kuvuna bila kupanda? Are they serious? Kwamba wategemee kuwekewa na Wajerumani na bado wapate pato wanaloistahili? Hilo jengo la ghorofa tatu ni sawa na mishahara yao ya siku ngapi? Na bado wanasema wanaipenda nchi. Si wangejitolea siku hizo (kama sio moja na nusu kwa kila mbunge) kuchangisha pesa za kumrudisha mjusi huyo?
Oooohhhh Lord have mercy on us.
Hivi tufanyeje kuwarekebisha hawa watu? Hivi kuna siku nchi itageuka na kuwaona hawa wanayoyafanya kweli? Hivi kuna siku mtu atakaa na kuihudumia nchi kwa manufaa ya nchi kweli?
NAACHA

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads