Wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wameanza kuumbuana huku kesho ikiwa ndiyo siku wanayoanza mkutano wao mkuu wa uchaguzi.
Hali hiyo ya kuumbuana ilitokea jana Dar es Salaam, baada ya mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Kabwe Zitto, kuvunja ukimya na kusema viongozi wa chama hicho makao makuu ni ‘wachafu’ na wanakiharibu chama.
Sambamba na hilo chama hicho kimesitisha matokeo ya uchaguzi wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) uliofanyika juzi, kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa, kutokana na kuwapo sura ya ufisadi.
Mama huyo, Shida Salum, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Walemavu, alisema hayo baada ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa kufungua mkutano wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA).
Shida alisimama na kupewa kipaza sauti na kusema ofisi ya makao makuu ya CHADEMA itaharibu chama na kwamba anasikia aibu kusikia mwanawe akitajwa katika vyombo vya habari kuwa ni mmoja wa mafisadi ndani ya chama. “Mimi fomu ya Zitto niliifukuza nyumbani kwangu, Zitto si fisadi, hanunuliki na hawezi kununuliwa,” alisema Mama Zitto.
Alisema amekuwa ndani ya chama hicho tangu mwaka 1992 na anasikia aibu zinapoibuka taarifa kwamba mwanawe ni miongoni mwa mafisadi. Alisema amekuwa akifika makao makuu kila mara kuomba kuonana na Katibu Mkuu (Slaa) ili wazungumze juu ya viongozi wake ambao wanamharibia chama na wanaotaka kukigawa.
“Siwezi kumkataa Zitto, katika uchaguzi huu ofisi imeingiliwa, jirekebisheni, chama kimechafuka, hali ambayo inafanya watu kukiogopa,” alisema mama huyo huku akishangiliwa na wanawake waliofika kwa ajili ya uchaguzi huo.
Lawama hizo ndani ya chama hazikuishia hapo, kwani baada ya Mama Zitto kuzungumza, Mwenyekiti wa Wanawake wa Mkoa wa Dodoma, Sakina Sare, alisema kuna matatizo ya kiutendaji miongoni mwa viongozi wa makao makuu.
Alisema aliingia katika chama mwaka 1994 na kuwataka viongozi hao kuwasikiliza wanachama ikiwa ni pamoja na kupokea matatizo yao.
“Kwa mfano, leo tunakaa katika uchaguzi wa Baraza la Wanawake, wakati huohuo fomu za kushiriki uchaguzi hazikuwafikia walengwa, hazikupatikana,” alisema Sakina. Alisema ipo haja kwa makatibu wa mikoa kuangaliwa kwa makini, ili chama kisigawanyike au kutoa taswira mbaya kwa wengine.
Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu wa Wanawake wa Mkoa wa Kagera, aliyefahamika kwa jina moja la Ramlaza, alisema wanachama wamekuwa na manung’uniko mengi juu ya uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na kutopata fomu za ushiriki katika maeneo yao.
Alisema maeneo mengine fomu za wagombea zilichelewa hali ambayo inaonesha utendaji dhaifu kwa ofisi ya makao makuu ya chama.
Aidha, baada ya wanawake hao kutoa hoja zao, Dk. Slaa aliomba radhi, lakini akasisitiza kuwa kama shutuma zilizotolewa na Mama Zitto ni za kweli basi hata mwanawe ni mmoja wa viongozi wa chama hicho.
“Katika hili la Mama Zitto siwezi kusema lolote, mimi ni Katibu Mkuu, mwanawe Zitto ni Naibu Katibu Mkuu, hivyo kama anaushutumu uongozi wa chama makao makuu, hata mwanawe yupo katika kundi hilo,” alisema Dk. Slaa.
Hata hivyo alisema anajua wapo vijana ndani ya chama hicho, ambao wanatumiwa na mafisadi na kwamba atawafuatilia na kuchukua hatua dhidi yao kwani chama hakitaruhusu kuyumbishwa au kuwapo makundi. Awali akifungua mkutano huo wa Bawacha, Dk. Slaa aliwataka wanachama hao kutamka hadharani kama kuna mianya ya rushwa ndani ya chama hicho katika mchakato wa uchaguzi.
Alisema asiyetamka hadharani kama kuna sura hiyo, hizo zitakuwa propaganda za kisiasa na kwamba hawataondoka katika kupambana na ufisadi. Aidha, alisema chama kimeletewa taarifa za kuwapo kwa kitabu cha aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, marehemu Chacha Wangwe kwamba kinasambazwa na watu wa CCM.
Alisema yeye hana matatizo na kitabu hicho, lakini anahofia yaliyomo ndani kwa kuwa CCM ilianza kutoa Waraka wa Wangwe Julai 27 mwaka jana siku moja kabla ya kifo chake. “Kwa maana hiyo, CCM walijua fika kuwa Chacha angekufa? Na kwa nini waraka huo ulitolewa na ofisi ya Katibu Mkuu CCM Dodoma?” Alihoji Dk. Slaa wakati akiwaeleza wanawake hao kujihadhari kwa kuwa si kila mwanachama ni mwema.
Alisema hoja inapoingizwa ndani ya chama lazima wawe makini na waijadili bila kuonesha hali yoyote ya uzembe. Kuhusu uchaguzi wa Baraza Kuu la Vijana, alisema alipata taarifa juzi usiku saa 3 kwamba zimetokea vurugu hivyo wanahitaji ushauri. Alisema alizungumza na vijana hao wapatao 110 usiku na kwamba waliopiga kura ni 186 huku wakitoa malalamiko yao kadhaa.
Alisema miongoni mwa malalamiko waliyotoa vijana hao ni pamoja na kuwapo kwa sura ya fedha ‘kutembea’ ndani ya uchaguzi, wagombea kugawa karatasi za kupigia kura na idadi ya kura kuongezeka.
Dk. Slaa alisema kutokana na hali hiyo, ilibidi kuitisha kikao cha dharura huku akiwa amewashirikisha baadhi ya wazee ambao kwa pamoja walikubaliana kuufuta uchaguzi huo na ufanyike ndani ya miezi sita.
Alisema kuhusu waliodaiwa kuhusika na sura ya kugawa fedha watawachunguza ili kupata ushahidi kamili na kwamba pindi wakiwabaini watawachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo habari kutoka ndani zilidai kuwa mgombea David Kafulila alikuwa ameshinda na badala yake “wazee wa chama walipoona mgombea wao John Hecha ameshindwa, wakaamua kuchukua hatua hiyo,” kilidai chanzo cha habari.
Inadaiwa wagombea hao, wamegawana kambi ambazo zinaanza kujionesha dhahiri ndani ya CHADEMA moja ikiwa ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na nyingine ya Zitto.
Habari hii imepatikana kutoka katika gazeti tando la
HabariLeo.co.tz
0 feedback :