wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Saturday, May 30, 2009

TweetThis! Kuzama kwa meli ya MV Fatih ya Kampuni ya Seagul

Salma Said, Zanzibar

MELI ya mizigo inayomilikiwa na Kampuni ya Seagul, MV Fatih, imepinduka na kuzama katika Bandari ya Malindi, Zanzibar, usiku wa kuamkia jana huku maiti za watu watatu zikiwa zimepatikana zikielea na watu wengine 27 wamejiokoa katika ajali hiyo na mamilioni ya mali kupotea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Bakari Khatib Shaaban amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo ambapo alisema kwamba Meli hiyo ilikuwa tayari imeshafunga gati katika Bandari ya Malindi majira ya saa 4.00 kamili uski juzi usiku na abiria waliokuwemo walikuwa wanataka kushuka lakini ghafla ilipinduka na kuzama baharini.
[DSC_7752.JPG]Kamanda Shaaban alisema hadi jana mchana ni maiti za watu watatu tu ndizo zilizoonekana ikiwemo ya mtoto mdogo wa kiume, na watu wazima mwanamke na mwanaume ambao hawakuweza kufahamika majina yao kamili kutokana na hakna jamaa waliozitambua maiti hizo.

Waliookolewa katika ajali hiyo ni Machano Mkinai, mkaazi wa Mkwajuni na Kitiba Mussa Kitiba, Gamba mkoa wa Kaskazini Unguja, Halima Mussa wa Arusha, Hassan Omar, Maulid Abdalla, wote wa Kisiju Mkoa wa Pwani.

Wengine ni Fatma Ali Salum, wa Kinyasini Wete kisiwani Pemba, Hawa Juma Saleh wa Rukwa Tanzania Bara, Zainab Ali Kitiba, Tandale Dar es Salaam, Sharifa Hamad wa Wingwi Pemba, Ramadhan Juma Mohammed Tandale na Omar Khamis Mohammed wa Vinguguti Dar es Salaam.

Amesema baada ya kutokea tukio hilo polisi walitaka maelezo ya Nahodha wa Meli hiyo, Ussi Ali ambaye wanamshikilia kwa maelezo zaidi lakini lakini maelezo yake yanaonesha wasi wasi kwa jeshi la polisi kutokana na kuwepo utatanishi mwingi katika maelezo ya Nahodha huyo.

Kamanda Shaaban alisema kwamba awali Nahodha alisema katika meli yake kulikuwa na abiria 25 na wafanyakazi 13, lakini Polisi inatilia shaka taarifa hizo kwani yawezekana Meli hiyo ilibeba abiria wengi na mizigo hivyo wanaendelea kumhoji Nahodha huyo hadi hapo maelezo jeshi la polisi litakapopata maelezo ya kuridhisha kutoka kwa Nahodha huo.

“Jeshi la polisi halijaridhishwa na maelezo ya Nahodha bado hasa katika idadi za abiria alizozitoa lakini bado tunaendelea kumuhoji kwani hatujaridhika na taarifa yake” Alisema Kamanda huyo.

Kamanda Shaaban alisema jeshi la polisi bado na uchunguzi wa kina ili kujua chanzo cha ajali hiyo na haitosita kuwachukulia hatua wanaohusika na kuwataka wananchi kutulia na kuacha vyombo vya sheria kufanya kazi zao kwa wazi.

Hali katika Bandari ya Zanzibar baada ya ajali hiyo kutokea ilionekana kuwa katika kitahanani kikubwa kwa wananchi wakiwemo wafanyabiashara waliokuwa eneo hilo wakisubiri mizigo yao na jamaa zao jambo ambalo lilisababisha msongomano mkubwakiasi cha kuwafanya Polisi kuwatawamya kwa kurusha risasi hewani.

kuwapo kwa hali hiyo kulilifanya Jeshi la Polisi kuweka doria kali katika maeneo yote huku wakishirikiana na baadhi ya askari wa vikosi vyengine kutokana na baadhi ya vibaka kujipenyeza na kuanza kuvuna mali zilizokuwemo katika Meli hiyo.

Hata hivyo kazi za utafutaji wa maiti nyengine iliendelea kwa siku nzima ya jana baada ya wazamiaji zaidi ya 30 wa KMKM kuifanya kazi hiyo baada ya kuwasili saa 8.00 za usiku wa juzi.

Kazi hiyo baada ya kupatikana kwa maiti tatu ilisita kwa usiku huo na kuendelea tena jana asubuhi kuanzia saa nne ambapo waokoaji hao waliamua kutumia mbinu mbali mbali za kuwawezesha kuingia ndani ya meli hiyo lakini hadi saa saba mchana walikuwa bado hawajafanikiwakuingia ndani ya meli hiyo.

Akisimulia mkasa wa ajali hiyo kepteni aliyekuwa akiendesha meli hiyo, Ussi Ali Ussi, alisema wakati akiingia Bandarini ghafla aliona meli hiyo ikijaa maji na kulala upande wa kushoto.

Alisema alianza safari yake saa 10.00 kutoka Dar es Salaam na kuja Unguja ambapo aliwasili saa 3.30 usiku lakini akiwa njiani alipata tatizo la usukuni kutoenda vizuri akiwa karibu na kufika Bandarini hapo.
Akiendelea alifahamisha ndani ya meli hiyo alibeba mizigo yenye uzito watani 40, abiria 25 na wafanyakazi wake walikuwa ni 13 ambapo watatu aliwaona baada ya meli hiyo kuzama lakini kwa wakati huo wa usiku hakujua wapi walipo.
Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa viongozi waliofika katika eeo la bandari na Zanzibar kuonana na abiria waliookolewa na kushuhudia ajali hiyo.

Rais Karume aliwataka mafundi wanayoifanyakazi ya uokozi kuonakuwa wanajitahidi kuhakikisha kuitafuta miili zaidi kama bado imo ndani ya meli hiyo.

Katika bandari hiyo umati kubwa ulikuwa umesheheni huku mamia ya watu wakiwa wamekaa nje ya geti la gati wakitaka kuingia ndani kushuhudia jamaa zao na ajali hiyo ambayo jambo ambalo limesababisha msongamano mkubwa bandarni hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Mustafa Aboud Jumbe alimweleza Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha kwamba juhudi za uokoaji inaendelea kwa kushirikiana na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Polisi na wadau wengine wanaojitolea kusaidia uokozi huo.

Jumbe alisema bado ni mapema kuielezea serikali juu yahatua za kuweza kuchukuliwa zaidi kwa vile wameanza kuifanya kazi hiyo ambapo imekuwangumu kutokanana na meli hiyo kuwa na mzigo mkubwa kiasi ambacho kimekuwa kikiwapa usumbufu waokowaji.

Kutokana na kuwepo kwa umma wa wananchi katika eneo la bandari Shirika la Bandari liliamua kufunga milango yake yote ya Bandari hiyo kwa usalama wa watu huku waandishi wa habari wakipata kazi kubwa katika ufanyaji kazi zake kutokana na vikwazo walivyokuwa wakiwekewa katika eneo hilo.

Jumbe alisema kwamba baadae watajaza upepo Meli hiyo iliyozama kwa kutumia kifaa maalum ili mizigo na watu waliokuwepo waweze kuja juu ambapo kazi hiyo itafanywa baada ya maji kujaa kwani kwa wakati huo maji yalikuwa yanakupwa na kazi hiyo ingeshindikana kufanyika.

Waziri Kiongozi aliwataka Viongozi wa Bandari kuieleza Serikali ni msaada gani wanaohitaji ili kuweza kufanikisha uokoaji wa mizigo, watu na meli hiyo ambapo Shirika la Bandari lilisema limejipanga vyema kukabiliana na janga hilo.

Wakati shirika la bandari likitoa ahadi hiyo hadi sasa hakuna msaada uliopatikana wa kutoa maiti zilizokuwa ndani ya meli hiyo huku Rais wa Zanzibar akilitaka shirika hilo kuomba msaada shirika la bandari la dare s salaam kuja kusaidia kuwaokoa watu waliomo ndnai ya meli hiyo.

Habari zaidi kutoka kwa abiria walionusurika katika ajali hiyo wamedai kuwa ndani kulikuwa na watu wengi wanaokisiwa kufikia 100, lakini Nahodha wa Meli hiyo anapingana na idadi hiyo na kusisitiza kwamba meli yake ilikuwa na idadi ndogo ya abiria.

Halima Mussa mkazi wa Arusha ambaye amenusurika katika ajali hiyo alisema kwamba wakati tukio hilo linatokea alikuwa tayati ameanza kushuka ndani ya Meli hiyo, lakini ghafla aliona ikipinduka wakati ikiwa imefunga gati na baadae akiwa katika maji alijikuta ameshikilia kitu.

“Mimi namshukuru Mungu kwa sababu nilikuwa nashuka lakini ghafla nikajikuta nimo katika maji lakini baadae nikakamata kitu bila kukijua ni kitu gani nilichoshikilia na nikaaza kupiga mayowe ya kutaka msaada na huku nyuma yangu nasikia sauti nyengine watu wakiomba msaada kuna watu wlaiokuwepo katika maji ndio wakanisaidia kwa kunambia shikilia hivyo hivyo hicho kitu na kunitaka ninyoosha mikono ndio waliponiokoa na kunileta juu” alisema huku akihema Halima Mussa.

Watu waliofika katika bandari ya Malindi yameilaumu serikali kw akshindwa kushukua hatua za dharura za kuweza kukabiliana na shughuli hiyo ambapo ajali imetokea majira ya saa 4 usiku lakini hadi saa tisa ndipo waokoaji waliopofika huku wakiwa hawana vifaa vya uokoaji.

“Ni dharau za hali ya mwisho hii maana ajali tokea saa 4 usiku lakini hawa watu wa KMKM wanakuja sa 9 hawana chochote cha kuweza kuwasaidia kuokoa abiria matokeo yake wamekuja na kuondoka kwa kisingizio cha kuongojea maji yakupwe” amesema Ali Haji Mkaazi wa Jangombe ambaye ana jamaa yake katika meli hiyo.

Naye Kepteni Juma wa meli ya Sea Bus amesema ipo haja ya kuwa na timu nzuri ya waokoaji na diver ili waeze kuwaokoa watu pindipo inapotokea ajali kama hiyo kwani.

“Lazima tuwe na timu nzuri ya divers wasaidie kuokoa lakini pia tax force ni muhimu kuwepo kwa ajili ya maafa kama haya na kufuata madili ya kazi ni kitu cha lazima kwa sisi manahodha ili kunusuru maisha ya watu” alisema Kemteni huyo.

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwaambia waandishi kwamba alisema wakati umefika hivi sasa kuhakikisha inalifanyia kazi tatizo hilo ambalo linaweza kuathiri wananchi wengi kwa kuziwajibisha taatisi husika kwa vile meli hiyo tayari hapo awali ilipata hitilafu na kulazimika kushusha abiria katika Bandari ya Mkokotoni baada kupata maharibiko ikitokea Pemba.

maalim Seif alisema ipo haja kwa serikali hivi sasa kuvifanyia ukaguzi vyombo vya usafiri kwa kuona inatenganisha huduma kati ya vile vinavyotoa huduma baharini.

Meli hiyo ambayo inamilikiwa na Said Mbuzi imeelezwa kuwa ilibeba mizigo mbali mbali ikiwemo Trekta, gari mbili, magunia ya unga wa ngano, sukari, mchele, magunia ya viazi, ya nyanya, mifuko ya saruji, magodoro na bidhaa nyengine ambazo zote zimezama huku wajanja wakitumia nafasi hiyo kuopoa bagodoro na bidhaa nyengine na kukimbia nazo nchi kavu.

Tukio za kuzama kwa Meli hiyo ambayo uzamaji wake unafanana sana na ule wa MV Bukoba linatokea wiki moja tu katika kumbukumbu ya kuzama kwa MV Bukoba mwezi Mei mwaka 1999 ambapo watu kadhaa walifariki dunia na kweka historia ya Tanzania katika ajali mbaya za meli zilizowahi kutokea nchini.

0 feedback :

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads