FemAct - Mapambano dhidi ya ufisadi: Serikali isikilize maoni ya Wananchi
FEMINIST ACTIVIST COALITION
(FemAct)
C/O Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) S.L.P 8921 Dar es Saalam,Tanzania, Kituo cha Jinsia, Barabara ya Mabibo Mkabala na Chuo cha Usafirishaji (NIT) Simu +255 22 2443205; 2443450; 2443286 Selula: 255 754 784 050, Fax. 2443244, Barua Pepe info@tgnp.org, Tovuti www.tgnp.org
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
‘MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI: SERIKALI ISIKILIZE MAONI YA WANANCHI’
(FemAct)
C/O Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) S.L.P 8921 Dar es Saalam,Tanzania, Kituo cha Jinsia, Barabara ya Mabibo Mkabala na Chuo cha Usafirishaji (NIT) Simu +255 22 2443205; 2443450; 2443286 Selula: 255 754 784 050, Fax. 2443244, Barua Pepe info@tgnp.org, Tovuti www.tgnp.org
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
‘MAPAMBANO DHIDI YA UFISADI: SERIKALI ISIKILIZE MAONI YA WANANCHI’
Sisi asasi za kiraia zaidi ya hamsini (50) wanaharakati tunaotetea usawa wa jinsia, haki za binadamu, ukombozi wa wanawake na maendeleo (FemAct) tulikutana tarehe 20 Mei 2009 kujadiliana kuhusu suala la ufisadi. Tumeguswa na kuchukizwa na mwenendo wa kushughulikia matukio ya ufisadi na ukwapuaji wa mali ya umma ambao umeendelea kushamiri kwa muda mrefu hapa nchini. Kushamiri kwa ufisadi kunabainisha jambo moja kubwa na lenye kutia mashaka; kwamba dola ya Tanzania tayari imetekwa na mafisadi. Kutekwa kwa dola kunaashiriwa na Serikali kusita-sita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya ufisadi na mafisadi, sera na sheria za nchi kubuniwa kwa malengo ya kunufaisha watu wachache, na viongozi wa kisiasa kupatikana kwa njia ya rushwa.
Wana-FemAct tunatambua na kuamini kuwa ufisadi ni vitendo vyote vinavyoambatana na kupora mali ya umma, kutumia madaraka vibaya, rushwa katika uchaguzi, mikataba ya siri ya uwekezaji na manunuzi, ulaghai katika kubinafsisha mali ya umma, kutumia fedha za umma bila kufuata vipaumbele vya taifa, uzabina-zabina katika kutekeleza sheria na sera za nchi, na kukiuka maadili ya uongozi wa umma.
FemAct inazingatia matukio kadhaa kubainisha na kuthibitisha ushamiri wa ufisadi nchini Tanzania. Ni matukio ya kashifa za ufisadi katika mikataba ya madini (mfano: Buzwagi); mikataba ya nishati (mfano: Richmond/Dowans, Independent Power Project –Tanzania Limited/IPTL); mikataba ya ubinafsishaji wa ovyo wa mashirika ya umma (mfano: National Bank of Commerce/NBC, Kiwira Coal Mine, Tanzania Telecommunications Company Limited/TTCL, Kilimanjaro International Airport/KIA, Tanzania International Container Terminal Services/TICTS, Tanzania Railways Corporation/TRC); wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma (mfano: ujenzi wa ghorofa pacha za Benki Kuu ya Tanzania, EPA [Kagoda], Commodity Import Support/CIS, Debt Conversion Programme/DCP); rushwa kubwa katika manunuzi ya umma (mfano: vifaa vya jeshi, rada, ndege ya rais); wizi wa kutumia nyaraka za kughushi (mfano: Tangold, Meremeta, Deep Green); uporaji wa maliasili za taifa (mfano: samaki, mazao ya misitu, wanyama pori); uporaji wa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji (mfano: kilimo cha mibono[jatropha] - Rufiji, Kilosa); na ununuzi na usambazaji wa dawa/vifaa vya afya hatarishi kwa afya za wananchi.
Tumetathmini na kubaini kuwa kushamiri kwa ufisadi nchini kunasababishwa na kutekwa kwa dola (rushwa na fedha chafu katika uchaguzi); sera kuu ya uchumi ya soko huria/holela inayoendeleza ubinafsshaji na ulegezaji wa fedha na uchumi kwa faida ya mabepari/mabeberu badala ya maendeleo endelevu kwa wote; kutokuwepo msingi-endelevu wa utawala bora; ulafi na ubinafsi wa viongozi; wananchi kutokudai uwajibikaji; kuendelea kutumika kwa baadhi ya sheria za kikoloni na Katiba iliyopitwa na wakati; mfumo wa uongozi wa vyama vya siasa kutoa fursa ya kudhibitiwa na mafisadi; na Serikali kulea kundi la ‘wateule’ wasioguswa na sheria!
FemAct inaamini ufisadi na sera ya soko huria vimesababisha madhara makubwa kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na Serikali kukosa msimamo thabiti kutetea maslahi ya taifa; kuyumba kwa uchumi wa nchi; utumishi wa umma kugeuzwa daraja la kujipatia utajiri; mgawanyo mbaya wa mapato hivyo kuwapo pengo kubwa baina ya maskini na matajiri; kuongezeka kwa ufukara miongoni mwa wananchi walio wengi; kushuka kwa kiwango cha ubora wa huduma za jamii – elimu, afya, maji, barabara, umeme, usimamizi wa kutoa haki; kupanda kwa gharama za maisha kiasi cha wananchi wengi kushindwa kuzimudu; ukosefu wa ajira; kuhatarisha usalama na amani (ukatili wa kijinsia na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, hususan ujambazi); kuimarika kwa mtandao wa mafisadi; kuongezeka kiwango cha vifo visivyostahili hususan, ajali, wanawake wajawazito na watoto; udanganyifu/wizi wa mitihani na kushuka kwa kiwango cha elimu; na kufa kwa vyama vya ushirika, kudorora kwa kilimo, ustawi wa jamii na kuhatarisha uhakika wa chakula.
Ni kutokana na bainisho la madhara ya ufisadi nchini Tanzania, FemAct inatoa msimamo wake na kudai yafuatayo:-
1. Serikali ichukue hatua za haraka kuwafungulia mashitaka na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi.
Serikali iwajibike haraka: kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu Richmond; kutoa taarifa sahihi na za kweli kwa wananchi kuhusu tuhuma/kashfa zote za ufisadi; kuweka wazi mikataba yote ya uwekezaji; na kusimamia vyombo vya dola hususan polisi, ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa serikali, TAKUKURU na Usalama wa Taifa kuwajibika ipaswavyo wakizingatia weledi, uadilifu na kanuni za utumishi wa umma bila visingizio..
Wananchi wawajibike kubaini na kukataa kuwachagua wagombea na vyama vya siasa vinavyotoa rushwa kwenye uchaguzi ili kununua utumishi wa umma na vinavyojihusisha na ufisadi wa aina yoyote; kukataa kutekeleza maamuzi yote yaliyofikiwa na viongozi pasipo kushirikisha wananchi na kwa mujibu wa sheria; kuwa macho kulinda ardhi na raslimali zao kuporwa na mafisadi; kuendelea kuhoji na kufichua mafisadi na ufisadi bila woga; na kuendelea kuunga mkono wale wote wanaofichua ufisadi na mafisadi.
Mashirika binafsi yawajibike: kuzingatia sheria na kanuni za uadilifu katika shughuli zao, wakiweka mbele utu na maslahi ya umma; na kuwafichua wenzao wanaoshiriki vitendo vya ufisadi.
Asasi za kiraia ziwajibike: kutoshiriki kwa namna yoyote ile katika vitendo vya ufisadi; na kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi.
Vyombo vya habari viwajibike: kuendelea na kazi yao nzuri ya kuibua, kuhabarisha na kuelimisha wananchi kuhusu ufisadi na ukwapuaji/uporaji wa mali za umma; kutokukubali kutumiwa kupotosha wananchi wakati wote wa mapambano dhidi ya ufisadi; na kuendelea kutoa elimu ya uraia ili kujenga uwezo wa raia kuiwajibisha serikali.
Viongozi wa dini wawajibike: kujibainisha wanasimamia upande gani katika mapambano dhidi ya ufisadi na kuhimiza uadilifu kwa wananchi; na kuendelea kukemea matumizi mabaya ya madaraka/mali ya umma, uporaji wa raslimali za taifa na rushwa katika uchaguzi/utumishi wa umma.
Vyama vya siasa viwajibike: kutathmini mfumo wao wa kupata uongozi na kudhibiti watu wasiokuwa waadilifu kuingia katika utumishi wa umma kupitia vyama vya siasa.
Mashirika ya fedha ya kimataifa [IMF na WB] na wafadhili wawajibike kutolazimisha nchi maskini kutekeleza agenda za mashirika husika au kuweka masharti yanayoendeleza sera ya soko huria/holela.
Wananchi, asasi za kiraia na serikali tuwajibike kushiriki katika mjadala wa kitaifa kuhusu mfumo mbadala wa uchumi unaohakikisha wananchi wote wananufaika na kuwa na haki ya maisha endelevu/ajira bila aina yoyote ya ubaguzi, kijinsia, kikabila, kitabaka, kirangi, kiumri, kitaifa, kidini au ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na ulemavu, na virusi vya UKIMWI.
Imetolewa na FemAct na kusainiwa na
1. Tanzania Gender Networking Programme (TGNP)
2. Legal and Human Rights Centre (LHRC)
3. Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA)
4. Youth Action Volunteers (YAV)
5. The Leadership Forum (TLF)
6. Coast Youth Vision Association (CYVA)
7. Walio Katika Mapambano na AIDS Tanzania (WAMATA)
8. Tanzania Media Women’s Association (TAMWA)
9. Youth Partnership Countrywide (YPC)
10. Tanzania Human Rights Fountain (TAHURIFO).
11. HakiArdhi
12. Women Legal Aid Centre (WLAC)
13. Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT)
14. Tanzania Coalition on Debt and Development (TCDD)
22 Mei 2009
0 feedback :