wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Sunday, January 25, 2009

TweetThis! Ernest Makulilo aandika : Tanzania na dhambi ya ubaguzi wa rangi

TANZANIA NA DHAMBI YA UBAGUZI WA WA RANGI
 
Nimekaa na kufanya tafakuri ya kina kuhusiana na mauaji ya ndugu zetu zeruzeru (albino) yanayoendelea kuisakama Tanzania. Katika tafakuri yangu hiyo nimejaribu kuangalia mambo makubwa mawili, suala la kwanza ni dhana nzima ya ubaguzi wa rangi (racism/racial discrimination). Na suala la pili ni mauaji yenyewe ya zeruzeru.
 
Lengo la kutaka kuchukua dhana hii ya ubaguzi na vitendo vya mauaji ya zeruzeru ni kutaka kuangalia kama mauaji haya na manyanyaso haya ni muendelezo wa dhambi ya ubaguzi wa rangi au ni “uonevu” tu kama wanasiasa na viongozi wetu wasemavyo.
 
Binafsi nijuavyo ubaguzi wa rangi si suala la kusema huyu mweusi (Black) au huyu ni mweupe (Mzungu), na huyu ni wa rangirangi (coloured). Ukiangalia ubaguzi wa rangi uliokuwepo Afrika Kusini kipindi cha makaburu, watu walipangwa katika makundi kutokana na rangi zao, mweusi, mweupe na wa rangirangi. Na kila kitu lilipata “benefits” zake. Katika katika kumbi za starehe kulikua za watu weupe ambapo mtu mweusi haruhusini kuingia, na kuna sehemu zingine hata kutembea mweusi hakuruhusiwa akikamatwa na kufungwa jela na kipigo kikali. Pia ubaguzi kama huu ulikuwepo katika nchi nyingi za magharibi. Mtu mweusi hakuruhusiwa kukaa baadhi ya viti ndani ya basi, nakumbuka nimeona picha ambazo zikiandika ONLY BLACKS AND DOGS HERE. Hii ilikua hatari sana kwani mtu mweusi alinyimwa haki zake kutokana na rangi yake ya ngozi.
 
Baada ya kuangalia hayo yaliyotokea Afrika Kusini na nchi za magharibi kuhusiana na ubaguzi wa rangi. Nikaanza kuangalia maana halisi ya ubaguzi wa rangi ni nini. Je, ubaguzi wa rangi ni suala la kusema mtu huyu ni mweusi, mweupe, au wa rangirangi tu? La hasha, ni lazima mtu apangwe kutokana na rangi yake, na rangi hiyo imfanye au anakosa haki zake za msingi kutokana na rangi hiyo. Na hata ukisikiliza kwa makini I HAVE A DREAM SPEECH ya Dr. MLK Jr, ilikua inaweka wazi kuwa walichokua wanataka ni mtu kuthaminiwa utu wake, mtu kutambuliwa kwa afanyayo na uwezo wake na si rangi yake imfanye akose mambo ya msingi, ateswe, atengwe nk. Leo hii tumeshuhudia ndoto ya Dr. MLK Jr, imetimia…sit u kwa Obama kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, la hasha bali watu katika mataifa ya magharibi wanaheshimiwa, kutambuliwa kutokana na utu wao, uwezo wao wa kufanya mambo na si suala la rangi tena.
 
Tanzania kwa kipindi hiki inakumbwa na mauaji ya zeruzeru kwa kasi kubwa ya ajabu. Imefika kuwa zeruzeru ameondolewa utu wake, amekua bidha adimu nay a gharama kubwa, zaidi ya kipindi cha utumwa. Serikali inachukua hatua mbalimbali, zingine ni za kufurahisha kuwa hazina msingi wowote zaidi ya kukurupuka. Mfano mpango wa serikali kugawa simu za mkononi kwa zeruzeru wote ili wakitaka kukamatwa wapige simu polisi. Sasa najiuliza, je hili suala la simu, je simu hiyo inachajiwa na teknolojia gani?Maana vijijini napo kuna zeruzeru na huko hakuna umeme, sasa itakuaje? Na pia tayari hizi simu zitakua ni kivutio kingine kwa zeruzeru kuvamiwa kwani kila mtu atajua zeruzeru ana simu, hivyo hata majambazi, wachuna ngozi, na wakata viungo vya zeruzeru kuongeza, huo ni mtazamo wangu tu.Na pia kipindi hiki tumeshuhudia serikali imefuta leseni za waganga wa kienyeji kama suluhisho. Je, ni kweli kama serikali isemavyo kuwa wanaosababisha mauaji ya zeruzeru ni waganga wa kienyeji au hata waendaji kwa wagnaga hao, hususani vigogo wenyewe wanaotaka vyeo vikubwa zaidi na utajiri mkubwa zaidi. Hili tuliachie hapo.
 
Ngoja tujiulize hivi zeruzeru (albino) ni mtu gani?Anaweza tambuliwaje kwa muonekano wake? Sintopenda kwenda ndani sana kwenye masuala la kibaolojia kutoa sababu za kuzaliwa kwa zeruzeru. Kwa kumtambua zeruzeru haijitahi uwe na microscope au elimu kubwa sana ya masuala ya kisayansi. Zeruzeru kwa kumuangalia rangi ya ngozi yake unaweza kumtambua.Zeruzeru ni mwafrika lakini si black kama wengineo, sasa sijui ni wa rangirangi (coloured) au la.
 
Swala la msingi ni kutaka kujua sasa je, mauaji haya ya zeruzeru nayo yamo katika kundi la ubaguzi wa rangi au la???? Binafsi naamini bila kipingamizi chochote kuwa mauaji haya ya zeruzeru ni ubaguzi wa rangi (racism) kama uliotokea Afrika Kusini, Marekani na nchi zingine za magharibi, lakini huu ni mkali zaidi. Nasema huu ni mkali zaidi kwani umelenga zaidi katika kuondoa maisha ya mwanadamu mwenzake kwa ukatili wa kunyofoa viungo, tofauti na ule wa kumzuia mweusi kutembelea mitaa flani au katika upandaji wa mabasi nk.
 
Kitu kingine cha kushangaza na kujiuliza, je kwanini Tanzania au watanzania kwa ujumla hatusemi ukweli kuwa mauaji ya zeruzeru ni ubaguzi ili tuweze kupambana nao ipasavyo, na jumuiya za kimataifa ziweze kutoa msaada wake?? Kwa mtazamo wangu, watanzania wengi tumeaminishwa kuwa sisi ni bora kuliko taifa lingine lolote lile kitamaduni na kimaadili…kumbe sio hivyo, si kweli. Kitendo Fulani kikifanywa na taifa mfano la Burundi, Kongo, Afrika Kusini, Ujerumani, Marekani nk tunasema ni ubaguzi wa rangi, unyanyasaji nk..kwa ujumla tunawanyooshea kidole kuwa wamepotoka. Je, mbona kitu hichohicho kikitokea Tanzania hatutaki kuweka wazi tunaanza kutafuta majina mengine kama unyanyasaji wa albino nk? Au kwani maana ya ubaguzi wa rangi, kitendo ni lazima kifanywe na mtu mweupe (mzungu) dhidi ya mweusi (mwafrika) hususani? Au hata mtu mweusi akimfanyia kitendo cha kumtenga mtu mweupe na kumnyima haki zake, kumnyanyasa kutokana na rangi yake ya uweupe nacho ni kitendo cha ubaguzi? Na kitendo cha mtu mweusi pia kumfanyia kitendo cha kumbagua mweusi mwingine kutokana na rangi yake (mfano mweusi sana/ mweusi tiiii na mweusi Fulani) nacho ni kitendo cha ubaguzi pia au? Au mweupe (mzungu) akimbagua na kumtenga, kumnyanyasa mweupe mwingine kama vile mwarabu, mchina nk nacho ni ubaguzi wa rangi???? Kweli hapa ndio penye kufahamu nini ni nini hasa. Mimi naamini ubaguzi haina maana lazima iwe kwa mweupe afanye kitendo hicho dhidi ya mweusi…lakini mweusi akifanya dhidi ya mweupe au coloured kisitafsiriwe kuwa ubaguzi
 
Nachojuwa mimi kwa kuangalia baadhi ya matukio yaliyokua yanatokea barani Afrika, mfano kipindi ambacho watu wa Afrika Kusini walipoamua kuwapiga na kuwaua kinyama wahamiaji waliopo kule toka nchi zingine hususani za Afrika, Tanzania ilikua ni nchi mojawapo iliyotoa tamko kali, na kwa uwazi kabisa kutamka “dhambi ya ubaguzi Afrika Kusini bado inawatafuna”. Nikaanza kuangalia mambo mengine ambayo ninayaona huku Marekani, mtu mfano akifanyia kitendo Fulani, akiwa ni mweupe kakifanya, anakimbilia kusema ni ubaguzi wa rangi. Sasa mimi najiuliza, je endapo mtanzania mweuzi mmoja akaenda nchi yoyote moja ya magharibi kama vile kusoma au kufanya kazi, na mtanzania huyo akauliwa na viungo vyake kunyofolewa kama anavyofanyiwa zeruzeru, je Tanzania itasemaje? Haina ubishi kabisa, kila mtu atasema mtanzania huyo mweuzi kabaguliwa kutokana na rangi yake. Sasa swali la msingi, je kitendo cha zeruzeru kunyofolewa viungo vyake kinyama, na hatimaye kuuliwa na mtu mwenye rangi nyeusi kisa rangi yake ni tofauti na mtanzania mweusi, je kwanini kisiwe kitendo cha ubaguzi wa rangi?Maana zeruzeru naye anatambulika kwa rangi yake ya ngozi, kama ilivyo kwa mweusi mwingine atambuliwavyo.
 
Kama tupo katika hatua hii tuliyoifikia ya kuweza kuuana kutokana na rangi zetu, moja ni nyeusi, na nyingine ni ya rangi (coloured)..wote ni binadamu, na ni watanzania..tunaelekea wapi wandugu? Hivi imefikia wakati zeruzeru inabidi asitembee peke yake, aitembee baadhi ya mida ikifika hasa jioni maana anachukuliwa kama “bidhaa”. Hadi mbunge maalum ambaye ni zeruzeru anapewa ulinzi binafsi asije uliwa na kunyofolewa viungo vyake. Je, mgombea urais 2010 akiwa ni zeruzeru watu tupo tayari kumpatia urais endapo atakua na sifa zote za kuongozi? Au rangi ya ngozi yake itaendelea kumtafuna kwa kuhesabiwa “bidhaa” muhimu?
 
Nini kifanyike kuondokana na dhambi hii inayotutafuna ya ubaguzi wa rangi????
 
TAFAKARI, CHUKUA HATUA DHIDI YA UBAGUZI HUU WA RANGI
 
NAWASILISHA HOJA
 
MAKULILO Jr,

2 feedback :

Luwilo said... Mon Jan 26, 02:34:00 AM MST  

kaka hapa hakuna lolote ni UBAGUZI tu na tena inavyoonekana kuna kitu hapa kimejificha tu ambbacho watu wantakiwa waweke wazi ili watu waelewe.
kwani serikali huwa haishindwi jambo hivyondo tunavyo amini na sometimes ni kweli.
swali sasa 'iweje serikali ishindwe kuwapata wale wanao ua albino??? na kama wakipatwa wanahukumiwa na kipengele gani cha sheria. we have to realistic here,muuaji ni muuaji tu haijarishi kamuua mtoto, mgonjwa au kamuua albino.he/she has to be treated like any other murderer

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads