Si Mganga lakini ni Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa
Katika hali inayoashiria kuwa bado maamuzi na utekelezaji wa mipango nchini Tanzania inafanywa katika mtindo wa 'zimamoto' na hivi kusababisha tujiulize ikiwa kweli watu waliopewa dhamana za uongozi wanazingatia taratibu za kazi, inaripotiwa kuwa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imemteua Kasimu Thadeo mwenye sifa za Uhandishi wa Afya ya Mazingira (Sanitation Engineering) kuwa Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa (DMO) baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Dk. Nasoro Rwabudongo kufariki dunia.
Sifahamu Katiba na muongozo unasomekaje kuelekeza nini kifanyike pale anayeshikilia nafasi fulani anaposhindwa kutimiza majukumu hayo ikiwa ni pamoja na hali ya ugonjwa, kifo, dharura ya kimasomo nk. Je! Ni faida ama hasara gani ingetokea kwa kiti hicho kuachwa wazi bila kaimu hadi pale ambapo angepatikana mtu mwenye sifa kamili za kushikilia usukani? Lakini hii pia inaashiria ni kwa kiasi gani Taifa lina wasomi wachache wa nyadhifa mbalimbali hasa afya katika maeneo ya vijijini. Malipo yasiyokidhi japo hata nusu ya haja za kimamaisha, huduma hafifu na mazingira duni ya kazi yamesababisha watu wenye taaluma mbalimbali wasiwe na msisimko ama wakate tamaa ya kutaka kuishi maeneo ya vijijini.
"Thadeo hana taaluma ya afya na wala si daktari kama anavyoitwa ingawa alipewa nafasi hiyo katika mazingira ya kufahamiana na baadhi ya watendaji wa manispaa na kwa kuwa hana taaluma ya afya, amekuwa akiendesha mambo kinyume na taratibu za afya".
“Ni kweli mimi si daktari. Nilikaimishwa ofisi hii baada ya daktari aliyekuwepo kwenda masomoni na kabla ya kurudi akafariki dunia akiwa huko na baada ya hapo nikaendelea kuwa DMO kwa sababu nina taaluma ya usafishaji 'cleanliness' na hii ilitokana na utaratibu wa ofisi hii kuwa na vitengo viwili ambavyo ni kitengo cha kinga na tiba ambalo ndilo eneo la daktari na eneo jingine ni la usafishaji ambalo ndilo eneo langu, hivyo mimi nikawa kama msimamizi wa masuala ya usafi na si masuala ya kinga na tiba."
"Sijashika nafasi hii kimakosa na wala kazi zangu haziendani na matibabu, hivyo nitaendelea kushika nafasi hii mpaka serikali itakapoleta mtu atakayeshika nafasi hii. Mimi nimeishika nafasi hii kama mtawala. Kazi ninazofanya ni za utawala tu lakini kazi zinazolenga masuala ya taaluma ya udaktari ninawatumia madaktari wa manispaa na wala mimi sichomi sindano wala siendi hospitalini.”
Alisema anafanya kazi kwa karibu na madaktari wa manispaa.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mstahiki Hassan Mwendapole anasema:
"Ni kweli huyo bwana hana taaluma ya afya na wala si daktari, bali ana taaluma ya afya ya mazingira na ni mtu pekee mwenye elimu ya chuo kikuu katika idara ya afya, hivyo tuliamua tumpe nafasi hiyo kwa sababu nafasi kama hiyo haiwezi kushikwa na mtu asiyekuwa na elimu ya chuo kikuu".
Alipoulizwa kwa nini wasichukue daktari kutoka katika Hospitali ya Mkoa ili aweze kushika nafasi hiyo, alisema: "Ni kweli tungeweza kufanya hivyo na kwa kuwa umenipa ushauri mzuri nitalifanyia kazi ingawa tulishaomba daktari mwenye elimu ya chuo kikuu aje kushika nafasi hiyo."
Kuhusu malalamiko ya wataalam wa afya kuwa Thedeo anakiuka kanuni na taratibu za taaluma ya afya tangu aliposhika nafasi hiyo alisema: "Mimi sina taarifa hiyo ila nitalifanyia kazi haraka iwezekanavyo."
2 feedback :
Kweli kati ya Kuku na Yai kipi kilianza. Haya hapa anayeteua m'kaimu ni nani? Manispaa yenyewe? Nas kweli aliomba mtaalamu wakanyimwa? Kwani hawa wanafanya kazi huko wilayani kutokana na uzawa ama wanapangwa na serikali? Maana alivyosema kuwa "ni mtu pekee mwenye elimu ya chuo kikuu kwenye idara ya afya na nafasi hii haiwezi kushikiliwa na mtu asiye na elimu ya chuo kikuu" ni kama vile hakuna mwenyeji wa hapo aliyemaliza Chuo Kikuu. Si wanahitimu huko na wanapangiwa vituo na serikali? Kwani ni wapi penye wagonjwa zaidi ambapo wahitimu wote wanapelekwa na ni uwiano gani hutumika kusambaza watu muhimu kama madaktari?
Sijui nani mwenye lawama, kati ya aliyeteua na aliyekubali wadhifa usiomfaa lakini najua kuna wa kulaumiwa katika hili.
Tuombe tu Mungu maana yasije yakatokea yale ya Dodoma (nadhani ilikuwa Dom) ambako mtu alichomolewa chumba cha upasuaji alipogundulika kuwa hana ujuzi wala elimu ya upasuaji. Sijui nini kingefuata.
Blessings
kukaimisha vyeo ktk SISIEMU au Vyeo vya kisiasa huwa hawakosei, ila ktk taaluma nyeti wanaweka kivuli ili waendelee kufisadi bila kipingamizi.