Vigogo wengine 4 wa BoT wafikishwa mahakamani Dar
Vigogo wanne wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kushtakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002 kwa shitaka la Uhujumu Uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh104 Bilioni.
Wakurugenzi hao wanashtakiwa kwa makosa tofauti ikiwamo kosa la tatu linalowahusisha wote wanne ambao ni Mkurugenzi wa Benki ya BoT, Simon Eliezer Jengo, Naibu Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo Kisima Thobias Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Bosco Ndimbo Kimela na Mkurugenzi wa benki, Ally Farijallah Bakari.
“Kwa pamoja na kwa makusudi walishindwa kuchukua tahadhari au kusahau majukumu yao katika mazingira nyeti, kwa udanganyifu walitayarisha nyongeza kwenye mkataba wa 2001 unaohusiana na uchapaji wa noti za benki kwa gharama kubwa ambapo bei ya mkataba huo iliisababishia serikali hasara ya Sh104,158,536,146,” alidai Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TaKuKuRu), Benny Lincoln alimwambia hakimu Samuel Maweda. Mbali na hiyo, pia Bw. Jengo alidaiwa kutoa amri ya uchapishaji wa noti nyingi zaidi ya kiasi kilichokuwa kinatakiwa na idara ya sarafu.
Lincoln aliendelea kuieleza mahakama kuwa mwaka 2004 washtakiwa Jengo na Mkango wakiwa ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam na wakiwa wameajiriwa katika utumishi wa umma katika nyadhifa tofauti ndani ya BoT, kwa pamoja na kwa makusudi, wakiwa na lengo la kuvunja kanuni walitangulia kutoa ofa kwa wasambazaji wa noti za benki.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo inatakiwa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo ndiyo ina mamlaka ya kesi za uhujumu uchumi.
Kwa upande wa mawakili wa washitakiwa ambao ni, Bw. Mpare Mpoki na Bw. Mabere Marando walipinga kufunguliwa kwa mashitaka mahakamani hapo kwa kudai kuwa kifungu cha 65(1) cha sheria ya BOT kinatoa kinga kwa wafanyakazi wa BoT kushitakiwa kwa kitu chochote wanachofanywa wakiwa wanatimiza majukumu yao kazini. Akiwasilisha hoja hizo Bw. Mpoki alisema kuwa mashitaka yote wanayoshitakiwa nayo washitakiwa hao ni makosa ambayo yamefanyika wakiwa kazini hivyo kutokana na kifungu hicho hawakustahili kushitakiwa.Mbali na hiyo alisema kuwa, Kesi hiyo imepokelewa kwa makosa mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka hayo hivyo wakaomba kesi hiyo ifutwe. Upande wa mashitaka ulipinga vikali hoja hizo na kudai kuwa mashitaka hayo yamefunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi ambapo iko wazi na inaelekeza mambo ya kufanya hivyo wakaiomba mahakama kutupilia mbali hoja hizo. Kutokana na kuwasilishwa kwa hoja hizo, Mahakama iliahirisha kesi hiyo na kuamuru washitakiwa hao warejeshwe rumande hadi Septemba 18, mwaka huu ambapo itatoa uamuzi juu ya hoja zilizowasilishwa baada ya kupitia na kuona sheria zinasemaje kuhusiana na jambo hilo - Majira.co.tzHabari hii kwa kina zaidi inapatikana katika gazeti tango la Mwananchi.co.tz
0 feedback :