Mwanasheria ICTR akutwa amekufa mezani, sebuleni!
Habari imeandikwa na Richard Konga kutoka Arusha wa gazeti la Majira.co.tz
MWANASHERIA wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji Rwanda (ICTR), Bw. Shyamlal Rajapaksa (42) raia wa Sri Lanka, amekufa katika mazingira ya kutatanisha ndani ya nyumbani yake eneo la Naura, Daraja mbili mjini hapa.
Kifo hicho kinadaiwa kutokea juzi saa tano usiku . Taarifa zaidi zinasema kabla ya hapo ,watu wawili mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Alifa, walifika nyumbani kwake na kabla ya kuingia, waliwasiliana naye kwa simu na kuamuru mlinzi awafungulie. Mlinzi huyo aliyefahamika kwa jina la Bw. Tumaini Lukumay, aliwafungulia na kuingia ndani kisha kuanza kunywa pombe na kubadilishana mawazo kwa zaidi ya saa tatu. Ilipofika saa 5:30 usiku, vijana hao walitoka na kumuaga mlinzi huyo ambaye alifunga mlango na kurudi kuendelea na lindo bila kujua chochote kilichoendelea ndani ya nyumba hiyo.
Asubuhi, msaidizi wa ndani aliyetajwa kwa jina la Bi. Joyce David (36) alifika kuanza kazini na kumkuta mwanasheria huyo akiwa amelala kifudifudi sebuleni na kutokwa damu puani na mdomoni. Alitoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi, ndipo walikwenda na kuchunguza eneo la tukio kabla kuchukua mwili huo kuupeleka Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Polisi walipoingia ndani, walikuta chupa za pombe aina ya Konyagi na baada ya kuchunguza, waligundua unga unaosadikiwa kuwa dawa za kulevya pamoja na bangi. Walichukua vitu hivyo pamoja na simu ya kiganjani ya marehemu kuvipelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Bw. Basilio Matei, amethibitisha kutokea kifo hicho na kueleza kuwa atatoa taarifa kamili baada uchunguzi kukamilika.
0 feedback :