wavuti.com Updates

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Napenda kuwataarifu kuwa blogu hii inapumzishwa rasmi na tovuti mpya imezaliwa kwa jina www.wavuti.com

This is to inform you that this blog has been retired. A new website to take her place is up and running at www.wavuti.com

Wednesday, October 22, 2008

TweetThis! Hekaya I

Karibu uketi penye mkeka usikize hekaya za bi Mdadisi binti Nsipitwe
Kwa uoza unaonuka Tanzania ya leo, mwenzako yamenikaba mafutu, kusema si hoja, Tanzania ya leo imekuwa kama gharika il hali tuliahidiwa pepo jamani!Wacha na leo mie niseme tena. Kadhia gani hii mtu unawaza hadi ubongo unajiuliza ‘kulikoni’? Vidole mali yangu. Maneno piya hazina yangu nayo karatasi pepe nimejaliwa kuifahamu. Wacha niandike tu. Hao, waliopewa dhamana na kuaminishwa kutuongoza katika kuifanya nchi kuwa mahala pazuri pa kuishi wamejwa na unafiki na uzandiki, wasokuwa na haya hayawani limewakumba pepo la ubadhirifu, wizi, uonevu, dharau,uasherati, ushirikina na mambo ya dizaini hiyo na pepo hili yaelekea halipungwi. Ikiwa hivi ndivyo ilivyo, kuyawazia maendeleo chanya Tanzania ni bora na aliyeota ndoto za Ali Nacha japo kavujiwa na pakacha kalijua kosa lake asilirejee.We hebu unidanganye ni nchi gani hiyo iliyoendelea kwa kutojali elimu, afya na mawasiliano, na hasa yale ya barabara? Ipi hiyo embu mtu unitajie nianze kuipakua? Lakini, sijakata tamaa bado, nina imani inawezekana kuiendeleza Tanzania yetu. Wasomi na wenye uchungu wa kweli na nchi yao wakaamua kuingilia nyanja za uongozi, madaraka na ushirikishwaji katika mipango halisi ya utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali, ni nani atathubutu kutema pumba zake upenuni? LiSerikali limejawa na mijitu inayotunga mambo ya kusadikika na yasiyotendeka. Jitu linaandika halafu ukiliuliza, “ehee, ewe, hebu tuambiye, Je! haya uloyaandika, kweli tukikupatia vifaa unaweza kuyatekeleza? Ama basi Je! tukikupatia mtu ambaye utampa mafunzo na umwelekeze namna ya kuyatekeleza haya uliyoyaandika, unaweza?” Toa asilimia kumi, zangu niachie tisini, hakika yake hawezi. Umejitakiya kung’aziwa mimacho mfano wa mjusi kafiri aliyebanwa na bawaba za mlango!

Ndiyo, Tanzania tunashindwa kuendelea kama zilivyo nchi nyingine sababu motisha na heshima ya kazi hakuna. Tanzania ya sasa tunayofanya ni aidha, kwa kubahatisha au kwa uzembe! Tunazungumza kwa midomo lakini matendo yashuhudia unungu nungu mtupu. Hata msemo wa ‘bongo usanii’ hauna kasoro!
Watu hatupendi kufundwa na adabu zikatukaa tukaiheshimu nchi alotutunuku Rabani basi leo wacha na yatupate yanayotupata kama ya Binti Tarabushi!

Bila nidhamu ya kazi hatwendi kokote na tusidanganyane kwa maneno ya kalumati. Tukubali kuzimeza shubiri wakati mwingine ingawaje chungu, hiyo pia n’ dawa ati! Na huo ni ukweli! Hutaki? Teta na Wamatumbi.Ndiyo ati! Nchi zote duniani huenda zimelaaniwa kwa kuwa zina kiasi chake cha mahakaba, walevi, wezi, wazururaji, wachawi , wavivu na kadhalika, lakini bado nchi hizo zimeweza kuendelezwa na watu wake wakapata mahitaji yao muhimu;Ala wamewezaje? Si ni kwa sababu ipo heshima kazini? Ama ulidhani ni mzizi tena?
Hakika ya dunia hii, mimi nimeshajifundisha kuwa, heshima ya kazi imegawanyika mara mbili: Hiyari au Lazima.- Hiyari kwa sababu wapo watu wenye hulka ya kupenda kusoma, kujaribu na kuonyesha mafanikio bila kujali ujira wake, alimunradi, malipo yake yanatosheleza mahitajio yake makuu mfano malazi, mavazi, chakula, matibabu, usafiri, elimu yake, ile ya wanawe na ya familia yake. Sifa ya kutenda jambo na kuweza kuisaidia jamii kwake ni kigezo cha kumtosha akeshe na kufanya kazi. u kwa kukusweka kambini au kukufunga jela.Tunabaki kusema hawa wametenda dhambi, ni waasherati na wazinzi kama wa mifano ya Sodoma na Gomora, haya sawa, twawahukumu kama vile yetu safi sana, washikishwa ukuta wa kwetu na machangudoa wa kwetu wao wa modeli tofauti, eti? Yote hayo bado ukweli unabakia palepale kuwa tunaowaita wenzetu, si wenzetu. Hukubali?
We jaribu umwite mwenzangu. Utaambiwa, “Mwenzangu na nani?” Huo mng’ako, kwa aibu utasahau kajia ulikojipenyezea sura yako. Bado unabisha? Haya we. Ingawaje wao pia wana masikini wao, lakini ukubwa wa umasikini wa Tanzania utajaa vyungu vingapi ukilinganishwa na chungu kimoja kitakacho ujaza umasikini wa hao tunaowaita wachafuzi wa maadili? Hujagundua tu kuwa hayo ya uchafuzi wa maadili hufanyika baada ya kutimiza wajibu na kutenda kazi?
Wakati fulani nimewahi kuuliza kundi pepe fulani kuwa Serikali ya Tanzania inajiteteaje katika utoaji malipo ya mishahara kwa waajiriwa wake endapo haipimi utendaji kazi kwa misingi ya muda alipofika mwajiriwa kazini na matokeo ya kazi yake? Sikupata majibu. Anayefahamu tafadhali nelimisheni mshamba mimi. Kila leo kauli mbiu ya Serikali, “Fungeni mikanda”, ebo nasi kiki kiki shurti kuikaza hadi yanatutoka mapovu sasa! Hatuulizi ni lini tunapaswa kuifungua mikanda hiyo. Ebo, wepesi wa kuteta, “Mikanda hii inaumiza aah?” lakini wazito wa kuamua kitendo.Mi nimeshajiambia, mfumo unaotekelezeka na wenye ahueni ni ule wa kupima muda wa kazi na /au uzalishaji wa kazi. Tanzania si lolote si chochote, kama hatujui mfumo unavyotendeka jama, si tuwapeleke watu kusoma na kujifunza kutoka kwa wengine? Si ndiyo maana tukawa na wasomi na wataalamu wa uchumi na mambo ya uongozi bora! Ama! Kumbe hawa wanasoma na kuwapo kwa ajili ya nani - nchi za nje - si ndiyo? Halafu tunashangaa ati kwa nini nchi hizo zinaendelea! Mwe! Hatukulijua hili?
Endapo wasomi wanabezwa na kuvishwa vilemba vya ukoka na kuzibwa midomo, nchi itaendelea vipi?
Wandugu,
Zipo njia za kuleta mabadiliko Tanzania, lakini ili hizi zifanikiwe, hatuna budi kuondoa na kusafisha uozo uliopo sasa. Wazee wenye hekima wamebaki wachache na si wote walio wazee huwa na hekima ama hufaa kwa mashauri, wengine ni vyema kabisa kuachwa wakae kimya au wakawacha kupayuka na tusijali wala kuyatendea kazi yanayoyapayukwa, itafika tamati, watakaa kimya - aliyekuwa na hekima nimemsoma alishafariki JK Nyerere (Pumzika pema) na sijui aliyeibeba mikoba yake ni nani. Yeye (Pumzika pema) alijua majira ya kuzungumza na nyakati za kukaa kimya baada ya kuona si yote aliyowaza kuwa yanatekelezeka. Sawa, alikosea, kwani nani malaika hapa duniani? Yupi aliyepewa nafasi amefanya mazuri kumshinda yeye (Pumzika pema)? Kila mtu ana kasoro zake bwana we. Mimi na wewe vile vile utake usitake. Sote tumepungukiwa na unavyoendelea kubisha ndiyo unaendeleza umaamuma tu. Lililobakia tumejifunza mazuri tuyatumie na yale mabaya tusiyoweza kuyarekebisha tuyaache na twendage mbele. Mbona mbishi hivi lakini?

- Lazima (kundi kubwa) kwa sababu mfumo wa Serikali unajengwa kwa namna ambayo usipofanya kazi utashindwa kulipa kodi za maji, umeme, nyumba, mawasiliano n.k, hivyo, ni lazima ufanye kazi ili uweze kuishi, ikiwa hutaki utaishi kama ombaomba na sheria za nchi zitakusulub

Pia, vijana wahuni waliojazana katika maeneo makuu yanayohusu maeneeleo hawastahili kuachwa tu wawepo! Usiniongopee, mi najua unawafahamu kuwa hawafai, tena si kwa majina na ubini wao tu, kwani si umesoma naye? na yule mwingine si umefanya kazi naye? sasa na huyu si tumemsoma tokea akiwa anakuzwa! Kamwe hatuwezi kuweka mvinyo mpya kwenye viriba vikuukuu kisha tukafumba macho na kusema eti havitapasuka na kumwaika na kisha kuishia kupumbaza roho zetu badala ya kuwaza hasara inayokuja! Huo utakuwa ni ujinga usio na maelezo.
Ni kweli kuwa, haiwezekani kwa miaka michache kubadili sura na mwendo wa kila kitu lakini zipo nyanja kuu ambazo zikiwekwa sawa tu, sehemu nyingine pia zitatengemaa na mengi sana yatarekebika. Kwani hujawahi kuona kwenye mnyororo wa baisikeli ukitoa gololi moja baisikeli inazaa mwendo wa bata? Umeyaona mashono ya nguo iliyoshonwa wakati mkanda wa chereheani umekaza? Sasa jaribu kutoa gololi nzee na kuweka mpya na chache za zamani zilizo nzuri zipange inavyotakikana ujionee jinsi usukani unavyokuwa mwepezi wenyewe na safari ikawa mwendo mdundo? Hebu badilisha mkanda wa cherehani na uweke oili uone marinda yatakavyonyooka? Kosa la viongozi wa sasa ni kuendelea kutumia mfumo wa uongozi uliopitwa na wakati na kukataa kujaribu mawazo mapya ati kisa ni mazoweya halafu tunataka tuendelee - mwe - na kama mawazo yetu ni kuwaza ati mabadiliko ni sawa na dhambi ya mauti tusijaribu kuigusa, basi na kuendelea tuhesabu ni - kalaghabaho! Na woga huu ndio unaoendelea kutusababisha tusiendelee.
kulikoni
Eti watuaminisha kuwa Tanzania itapaa …. na siye tulivyo wepesi wa kuwaza tushajenga taswira kuwa tumo ndani ya dege lipaalo wakati hatuwezi hata kuiona tiara, wachilia mbali boingi…
Hadi hapo tutakapoamka, tukashikamana shime ili tuendelee…….
Miye Bi Mdadisi binti Nsipitwe wacha nende zangu nikatimize wajibu wangu…”Siasa si hasa, bali visa na mikasa”

5 feedback :

BLACKMANNEN said... Mon Nov 10, 05:03:00 AM MST  

Hi Bi Mdadisi binti Nsipitwe,

Maelezo yako mengi ni mazuri sana, lakini ni pointi moja tu ya maana uliyoitoa katika maneno yako hayo. “Kipimo cha kazi”.

Nakupongeza pia kwa kuielewa na kuitumia lugha ya kiswahili katika uandishi wako kiufasaha. Nimekuonea gere sana kwa hilo.

This Is Black…..Blackmannen!

subi said... Mon Nov 10, 05:03:00 AM MST  

BLACKMANNEN, Asante kwa kupoteza muda wako kusoma mbwabwajo wangu. Wakati mwingine inabidi kusema tu kama mwehu japo ipendeze kama hekaya, ikiwa kusema kwingi hakusaidii katika kubadilisha lolote. Iliyobaki basi ni bora tuyatungie hadithi na hekaya kama si porojo maumivu yetu.
Ama kweli KiSwahili ni lugha tamu sana utamu wake vigumu kuuonja kwa yeyote asiyependa kula!

Harold said... Mon Nov 10, 05:04:00 AM MST  

binti mdadisi, [Mana Mshiki] BIG UP,
Mimi binafsi yangu ninaomba nikipongeze kwa kazi nzuri unayoifanya. mimi ni mdau wa blogu zako kwa kweli ninajivuna kuwa na dada kama wewe. Keep it up. mimi nakubaliana na mawazo yako, umeongea mambo ya msingi sana. I wish ungeonwa ukaingia Bungeni kuongeza nguvu dhidi ya mafisadi.
ni hayo tu.
ni mimi [mchuku wa njama ya mangi]

subi said... Mon Nov 10, 05:04:00 AM MST  

Karibu mshikyi,
Mmbony tsapho?
Asante Harold kwa kupita hapa, muda na yale uliyoyaandika. Nitaendelea kuweka mawazo yangu katika maandishi japo ikiwa ni kwa kuburudisha maana ndiyo lengo kuu la tamthiliya, hekaya, riwaya, tungo na hadithi.
Karibu tena wawae!

Recent Comments . Kauli za Wasomaji

###recentComment###

More Opportunities ads